Hawa Ndiyo Wateja Wenye Faida Kubwa Kwenye Biashara Yako.


Image result for duka lenye wateja wengi

Wateja wa biashara yako hawafanani wala kulingana, lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wanawachukulia wataja wote wa biashara kama wanafanana na wako sawa. Hili limekuwa linawanyima fursa ya kunufaika zaidi na wateja ambao ni tofauti tofauti kwenye biashara zao.

Tukiwagawa wateja wa biashara yako, tunaweza kupata makundi mawili makubwa;

Kundi la kwanza ni *wateja wapya*, hawa ni wateja ambao ndiyo wanaijua biashara yako kwa mara ya kwanza, na ndiyo wamekuja kununua au hata hawajawahi kununua. Hawa ni wateja ambao unahitaji kuweka kazi kuwashawishi wanunue kwako, na unahitaji kutumia nguvu nyingi kuwaridhisha.

Kundi la pili ni *wateja wanaojirudia*, hawa ni wateja ambao walishanunua kwako mara kadhaa na wanaendelea kununua kwako. Hawa ni wateja ambao wameshaielewa biashara yako na wameshajua namna biashara yako ilivyo muhimu kwao na hivyo wanakuja kupata kile wanachohitaji.

Sasa ukiwalinganisha wateja hawa wa biashara yako, wale wapya na wanaojirudia, wateja wenye faida kubwa kwa biashara yako ni wale ambao wanajirudia. Hii ni kwa sababu huhitaji nguvu kubwa kuwashawishi wateja hawa kwa nini wanapaswa kununua, wameshajua unatoa thamani wanayoihitaji hivyo wanakuja kununua.

Lakini lipo kosa moja kubwa ambalo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya. Kosa hilo ni kuwahudumia wateja wanaojirudia kwa mazoea, kuona kwamba hawana pengine pa kwenda ila kuja kwenye biashara zetu. Hali hii imekuwa inatoa mwanya kwa wafanyabiashara wengine kutoa thamani kubwa zaidi ambayo inaweza kuwahamisha wateja wako.

Wateja wanaojirudia kwenye biashara yako wanaleta faida kubwa na pia wanawaleta wateja wengine wengi. Ni jukumu lako wewe kama mfanyabiashara kuhakikisha wateja wanaojirudia wanapata huduma bora kabisa. Kuwapa sababu ya kuendelea kuwa wateja wako na kuachana na wafanyabiashara wengine ambao wanawashawishi wakanunue kwao.

Waoneshe wateja wako wanaojirudia kwamba unawathamini, kwa kuwapa zawadi na ofa mbalimbali. Pia wafanye wawe tayari kuwaambia wengine kuhusu wewe, kwa kuwapa thamani kubwa sana ambayo hawakutegemea kupata na hata wakienda kujaribu kwa wafanyabiashara wengine hawawezi kuipata. 

@mapambano_

No comments

Powered by Blogger.